Thursday, May 11, 2006

Ndugu Mtanganyika

Ndugu Mtanganyika

Wednesday, May 10, 2006

Bendera ya Tanganyika, naamini kuwa itaendelea kutukumbusha utu wetu, uhai wetu na utajiri wetu. Hii bendera, iliishusha bendera ya mkoloni! ni alama ya ushindi wetu dhidi ya ubinafsi, unyonyaji na aina zote za unyanyasaji na udhalimu.
TULIPENDE TAIFA LETU; MUNGU AZIBARIKI TANGANYIKA, UNGUJA NA PEMBA

Mgombea Binafsi Sasa Ruksa Tena lakini Katiba bado ina.....

Nikipata nafasi baadaye nitazungumza kwa kina kuhusu suala la Mgombea Binafsi. Lakini kwa leo naona ni vema tukajikumbusha tu,
Katiba ya Kwanza ya Tanganyika [Tanganyika(Constitution)Order in Council, 1961 haikuwa inakataza mgembea binafsi. Baadaye mwaka 1962 Tanganyika ilipokuwa Jamhuri, katiba ya Jamhuri ya Tanganyika nayo haikukataza mgombea binafsi. Mgogoro ulianza mwaka 1965 pale Jamhuri ya Tanganyika ilipotungwa katiba ya Muda ya mwaka 1965 na kufuta kabisa mfumo wa vyama vingi na kutamka wazi kuwa mambo yote ya siasa katika Tanzania yatasimamiwa na TANU kwa upande wa Tanganyika na ASP kwa upande wa Zanzibar. Ibara ya 27(1) ya Katiba hiyo ya muda ilieleza kuwa : raia yeyote wa Tanzania aliyefikisha umri wa miaka 21 na ambaye ni mwanachama wa CHAMA... anaweza kugombea ubunge..." Hapo awali hakukuwa na sharti la kuwa mwanachama, lakini wakati huu likaingizwa katika katiba kwa lengo la "kuimarisha umoja wa kitaifa" na kuleta "maendeleo"! Ni ajabu kama umoja wa kitaifa unaimarishwa kwa kukiuka misingi ya haki za binadamu! hapo utatia akili mwenyewe.
Mwaka 1977 'ilipotengenezwa'Katiba ya Muungano na jopo la 'wataalamu' ishirini, baada ya TANU na ASP kuungana, hapo ikabainishwa kwa kukolezwa kuwa nchi itakuwa yenye kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea chini ya uongozi wa CHAMA [ibara ya 151 ya katiba ilitoa fasiri ya CHAMA kuwa ni 'Chama Cha Mapinduzi kilichotajwa katika ibara ya 3(3) na (10) ya Katiba hii'. Hali hiyo ikawa ni desturi mpaka pale wakina Mapalala na wenzake walipoanza kudai vyama vingi! Mabadiliko ya mwaka 1992 yakaleta mambo mapya kwa kuruhusu vyama vingi. hii ilikuwa ni kwa mujibu wa sheria namba 4 ya 1992
Pamoja na mabadiliko hayo kuruhusu vyama vingi, bado kukawekwa masharti chungu mbovu katika kuanzisha vyama vya siasa. Mchungaji mtikila akaamua kufungua shauri la kikatiba mahakamani akipinga kushurutishwa kuwa mwanachama ili aweze kupat haki ya kugombea katika kesi namba 5 ya mwaka 1993, ambapo Hayati Jaji Lugakingira alitamka kuwa ugombea binafsi ni ruksa na sheria yoyote inayokataza ugombea binafsi ni batili kwa kuwa iko kinyume cha katiba.
Mchezo wa kiaina ukaanza baina ya Mahakama na Bunge. Serikali ikapeleka rufaa mahakamani, kwa rufaa namba 3 ya 1995 lakini wakati rufaa ikaliko mahakamani mlikisubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa, serikali tarehe 16/10/94 ilikwishapeleka mswada haraka bungeni ili kurekebisha Katiba kwa lengo la kuingiza yale yote yaliyotamkwa na Jaji Lugakingira kuwa ni batili! Baada ya mswada kufikishwa Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akapeleka ombi mahakama ya rufaa akiomba kuondoa rufaa yake!
Hebu ona, huu ndio utawala wa sheria?
Nakumbuka kuwa Jaji Kisanga, akiwa kaimu Jaji mkuu wa Tanzania, alilalama kwa kusema kuwa serikali kwa makusudi imeamua kugoganisha Mahakama na Bunge kwa kuviomba vyombo vyote viwili kwa wakati mmoja kushughulikia jambo moja. Hali hiyo ni ya kujutiwa na kutubiwa.
Katika shauri la majuzi la kurejesha mgombea binafsi, Mahakama imelilaani Bunge kwa kukubali kufanya mabo kinyume na misingi ya utawala bora. Hata hivyo haya yote yanayotekea ni viashiria tu vya ubovu ulioko katika katiba. Mimi kama mtanganyikamzalendo nina mawazo haya:
a) Kuna Umuhimu Mkubwa wa Tanganyika na Zanzibar Kuwa na Katiba mpya:
Kumekuwepo na hoja kutoka kwa wadau mbalimbali kuwa katiba iliyopo ina mapungufu makubwa na haikidhi matakwa na maslahi ya wananchi kwa wakati uliopo kutokana na mabadiliko mengi ya kisisasa, kiuchumi na kijamii ambayo yamekwishatokea tangu katiba hiyo ilipotungwa mwaka 1977. Baadhi ya mapungufu yanayosemwa ni pamoja na katiba kulimbikiza mamlaka kubwa zaidi kwenye mhimili wa utawala kuliko mihimili mingine ya mahakama na Bunge na hivyo kutoa mianya ya ukiukwaji wa haki za binadamu, katiba kukidhi mfumo wa chama kimoja zaidi badala ya vyama vingi, Tume ya uchaguzi isiyo huru, uwiano mbovu wa kijinsia katika nafasi mbalimbali za uongozi. Aidha, katiba iliyopo inakosolewa kwa kupotosha umma kuhusu aina ya siasa na mfumo wa uchumi unaoliongoza Taifa kwa kuendelea kutamka kuwa Tanzania ni nchi inayofuata siasa ya ujamaa na kujitegemea wakati utendaji unaonyesha bayana kuwa mfumo wa uchumi wetu ni wa soko huria. Kuendelea kuweka viraka katika katiba mara kwa mara ni uthibithisho kuwa katiba iliyopo haikidhi haja na matakwa ya wananchi wake na wala mabadiliko yanayofanywa hayalengi kuifanya katiba iwe chombo cha kudumu. Hivyo basi upo ulazima wa kuandikwa kwa katiba mpya itakayozingatia matakwa na maslahi ya wananchi pamoja na mahitaji ya wakati. Kwa kuanzia, uwepo mjadala wa kitaifa kuhusu uundwaji wa katiba mpya ili kutoa fursa kwa wananchi na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuamua mustakabali wa taifa lao. Maoni yakishakusanywa yaridhiwe kupitia mkutano maalumu wa katiba (badala ya Bunge kama ilivyozoeleka) kwa mchakato unaokubalika wa utungaji wa katiba mpya kama inavyofanyika kwa nchi za Kenya na Zambia.

b) Mawaziri wasiwe wabunge:
Mfumo wa sasa ambao unampa mamlaka Rais kuteua Mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge wa chama kilichoshinda uchaguzi haufai kwavile unadhoofisha kabisa dhana za uwakilishi, uwajibikaji na mgawanyo wa madaraka (separation of powers) kati ya mihimili mitatu ya dola ambayo ni Bunge, mahakama na Utawala. Kwa kawaida, ili wabunge waweze kufanya kazi zao za uwakilishi wa wananchi, kutunga sheria na kuiwajibisha serikali kikamilifu, hawapaswi kupewa nyadhifa katika serikali wanayopaswa kuiwajibisha kwavile si rahisi kuiwajibisha serikali ya chama chao mbele ya wapinzani. Aidha, Mbunge akiteuliwa kuwa waziri anawanyima wananchi wake haki ya kuwakilishwa na kuihoji serikali kutokana na kanuni ya uwajibikaji wa pamoja wa mawaziri (collective responsibility) ambayo inawalazimu mawaziri wote kuitetea serikali. Muunganiko huu wa madaraka ya kiuwakilishi na kiutawala ni mkanganyiko wa kimfumo ambao unadhoofisha nguvu ya Bunge na kulifanya muhuri wa kupitisha maamuzi ya serikali hata pale yanapokinzana na matakwa ya wananchi wanaowawakilisha. Inapendekezwa kuwa Rais apewe mamlaka ya kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa watu wenye sifa hizo katika jamii ili wabunge wabaki kuwa wawakilishi wa wananchi tu. Mfumo huu utaongeza uwajibikaji wa serikali kwa Bunge na wananchi na kuboresha utendaji wa bunge na uwajibikaji wa wabunge kwa wananchi wanaowawakilisha.

c) Utaratibu wa wabunge wa kuteuliwa ufutwe:
Rais tayari ana mamlaka kubwa sana ya kiutendaji ambayo baadhi yake yamekuwa yakilalamikiwa kuwa yanakiuka misingi ya haki na demokrasia. Kwa vile Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, kinachokusanya wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, ni kinyume na misingi ya demokrasia kwa Rais kupewa mamlaka ya kuteua wabunge. Zimekuwepo hoja za msingi zinazodadisi kuhusu uwakilishi na uwajibikaji wa wabunge hao pamoja na vigezo vinavyotumika kuwateua. Je, wabunge hao wanamwakilisha nani au ni jimbo lipi wanalolitumikia? Je vyama vina nafasi gani ya kupendekeza majina (hasa kama ni vya upinzani) na kuwawajibisha wabunge walioteuliwa na Rais?

Kutokana na hoja hizo, inapendekezwa kwamba utaratibu wa Rais Kuteua wabunge ufutwe. Aidha inapendekezwa kuwa ni muhimu kwa Katiba kutoa nafasi za uwakilishi bungeni kwa makundi mbalimbali ya kijamii (kama vile vyama vya Kiraia, vijana, vyama vya wafanyakazi n.k) ambayo yamekuwa yakidai uwakilishi bila mafanikio.

d) Wabunge Wawajibishwe Katikati ya Mihula:
Kipindi cha miaka mitano tangu mbunge anapochaguliwa hadi atakaporudi kuomba kuchaguliwa tena ni kirefu mno hasa pale mbunge anaposhindwa kutekeleza wajibu na ahadi alizotoa kwa wananchi waliomchagua. Kwa kuwa katiba haina ibara inayoruhusu wabunge kuwajibishwa katikati ya muhula inapendekezewa kuwa: iwepo ibara itakayowapa uwezo wananchi kumwajibisha mwakilishi wao angalau baada ya miezi kumi na nane (18) tangu kuchaguliwa kwake ikiwa hawatakuwa wameridhishwa na utendaji wake. Pia itungwe Sheria itakayotoa utaratibu wa kufuatwa na wananchi katika kumwajibisha mbunge wao kwa mujibu wa kifungu hiki cha katiba.

e) Umri na Kiwango cha Elimu ya Rais:
Kiwango cha umri wa sasa wa miaka arobaini (40) kwa mujibu wa katiba ni kiwango kilicho juu mno ambacho kimekuwa kikilikosesha taifa hazina kubwa ya viongozi ambao hawajafikisha umri huo lakini wana upeo na uwezo mkubwa wa uongozi. Inapendekezwa kwamba umri wa mgombea wa nafasi nyeti kama hii ni vema ukawa miaka thelethini, umri ambao tayari historia imeonesha kuwa ni wakati mzuri zaidi wa kiongozi kuchapa kazi kwa busara, juhudi na maarifa ya hali ya juu. (mfano: Julius Nyerere, Fidel Castro, Amilca Cabral, Joseph Kabila n.k)

f) Fursa ya Ugombea huru/binafsi:
Mfumo wa chama kimoja ulikosolewa kwa kubana haki ya mtu kugombea uongozi. Pamoja na mfumo wa vyama vingi kudhaniwa kuwa umepanua na kuimrisha wigo wa demokrasia, mfumo huu pia unakosolewa kwa kuendelea kubana uhuru na haki ya mtu anayetaka kugombea uongozi bila kupitia tiketi ya chama cha siasa. Ili kutoa haki ya kweli kwa mtu kushiriki katika uongozi, Katiba itambue na kutoa fursa na haki ya ugombea huru/binafsi kama ambavyo wadau mbalimbali wamekuwa wakishinikiza.

g) Uhuru wa Kiongozi Kubadilisha Chama:
Licha ya kuzoeleka kwa mfumo wa kupata wawakilishi kupitia vyama, upo ushahidi kwamba moja ya mapungufu yanayotokana na mfumo huu ni kuwafanya wawakilishi wanaopatikana kupitia vyama vya siasa kutokuwa na uhuru wa kutosha kutoa maoni yao, hasa pale maoni hayo yanapokuwa yanakwenda kinyume na uongozi au sera za chama chao. Mfumo huu unawawajibisha zaidi wawakilishi kwa vyama vyao kuliko kwa wananchi waliowachagua. Ipo haja basi kwa katiba kutoa fursa kwa Wabunge, madiwani na wawakilishi wengine kuwa huru kubadilisha vyama pasipo kupoteza nyadhifa zao za uwakilishi. Hii itawahakikishia wananchi haki yao ya kuwa na wawakilishi na italipunguzia taifa mzigo wa gharama za kufanya chaguzi ndogondogo kila mwakilishi anapoacha au kuvuliwa uanachama na chama chake.

h) Adhabu ya Kifo/Haki ya kuishi:
Pamoja na kuwa madhumuni na sababu za marekebisho ya kumi na nne ya Katiba kuwa nikuondoa vifungu vyote ambavyo vinanyima au kubana haki na uhuru, bado Ibara ya kumi na nne cha katiba inaendeleza tatizo la kuiweka Katiba chini ya sheria nyingine ambapo haki hiyo msingi ya kuishi bado inaathiriwa na sheria zinazoruhusu adhabu ya kifo. Umefika wakati sasa wa Tanzania kufut adhabu ya kifo.

j) Sheria Mbaya Kuruhusiwa Kuendelea Kutumika:
Ibara ya 30(5) ni ibara ambayo inaruhusu sheria mbaya kuendelea kutumika kama vile ni sheria halali hata pale ambapo mahakama inakuwa imeng’amua na kuhukumu kuwa sheria hiyo imakiuka katiba. Ili kuboresha ulinzi wa haki za msingi zilizoainishwa katika Katiba, ni vema kifungu hiki kikafutwa.
Tuwasiliane tena wakati ujao:
napatikana kituo cha sheria na haki za binadamu, Dar es Salaam - Tanzania.

SALAAM NDUGU

Wanablogu,

napenda kuwasalimu na kujiunga nanyi katika mtandao huu.
mimi ni mmoja wa wanasheria wanaharakati wa haki za binadamu hapa Tanzania.
naamini tutawasiliana sana na kushirikishana mambo mengi mazuri

binadamu wote ni sawa
na afrika ni moja.